Sunday, October 16, 2016

Makamu Wa Rais Samia:tunaendelea Kuziba Mianya Ya Rushwa/wafichueni Wafuja Fedha Za Serikali

MAKAMU wa rais ,Samia Suluhu Hassan,amewataka kuwafichua watumishi mbalimbali wa halmashauri na taasisi za serikali katika wilaya na mikoa wanaodhaniwa kufuja fedha za serikali na kupoteza mapato lengo ikiwa ni kuzikusanya fedha na kuzirudisha katika mikono ya wananchi waone faida yake.

Amesema serikali ya awamu ya tano inaendelea na nguvu yake ya kukusanya mapato na kuziba mianya ya rushwa na kupotea kwa mapato.

Aidha Samia ametoa rai kwa wananchi mkoani Pwani kuendelea kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kulinda amani na usalama wa mkoa huo kufuatia  kujitokeza kwa mambo ambayo yameonekana kuhatarisha usalama wa mkoa hivi karibuni.

Katika hatua nyingine amewahakikishia wakazi wa mji wa Chalinze kutatua tatizo la maji ambalo bado ni kero kubwa ambapo ameeleza kwamba mwishoni mwa mwaka huu matunda yataanza kuonekana.

Akizungumza na baadhi ya wananchi wa Mlandizi na Chalinze,mkoani Pwani wakati aliposimama kuwasalimia akielekea mjini Dodoma kikazi,alisema wananchi waiamini serikali yao kwani imeanza kuirejesha nchi katika nidhamu ya mapato na matumizi na kazi ya maendeleo inaendelea.

“Watanzania watajenga Tanzania yao wenyewe na serikali yake na Tanzania inaweza kujiendesha yenyewe na kama itategemea misaada iwe sio kwa kiasi kikubwa.”alisema.

Aliwasisitiza wananchi kulipa kodi pale inapohitajika ili kusaidia na serikali kuinua mapato yake.

Hata hivyo Samia aliwataka wakulima na wafugaji kuishi kwa upendo na mshikamano baina yao pasipo kutofautiana kwani kwa kufanya hivyo kunasababisha migogoro isiyo na tija na wakati mwingine kuvunja amani.

Kufuatia ombi la Mbunge wa jimbo la Chalinze ,Ridhiwani Kikwete ,kumweelezea kuhusu kero ya maji inayowakabili wakazi wa jimbo hilo,Samia alisema serikali inatambua hilo na kwasasa ipo katika mpango mzuri wa kumaliza tatizo la maji lililopo.

Alielezea kuwa WAMI yapo maji ya kutosha lakini tatizo ni usambazaji ,hivyo wanatarajia kuvuta maji kwa mabomba hadi eneo la Pera na kujenga matanki makubwa yenye ujazo wa lita 300,000 ,Kibiki watajenga tanki lenye ujazo wa lita 200,000 ili maji yakifungwa kuweze kuwa  na maji ya kufikisha kwa wananchi kirahisi.

Makamu huyo wa rais alisema watajenga hifadhi nyingine ya maji pale Mazizi yenye lita mil.2 ambayo itawezesha kutumia maji ndani ya wiki mbili bila kukatika ambapo mpango huo upo njia na tayari mkandarasi yupo na wametanguliza sh.bil 43 ili kazi ianze .

Samia wakati anafanya kampeni ili kuomba kuchagulia kuingia madarakani aliahidi kuwatua akinamama ndoo kichwani kwa kutatua tatizo la maji na kusema anashughulikia suala hilo hadi hapo atakapowaondolea wananachi adha ya kutembea umbali mrefu kusaka huduma hiyo muhimu.

“Nayachukua mambo yote na nitaendelea kuyafanyia kazi ,natambua kilio chenu hasa akinamama ambao huamka usiku ama kutembea umbali mrefu kutafuta maji”alisema Samia.

Akizungumzia suala la afya kuhusu vifaa tiba alisema atazungumza na wizara husika kutatua kero ya vifaa tiba,madawa na watumishi katika kituo cha afya Msoga ili kupunguza mzigo kwa hospitali za rufaa ikiwemo Tumbi.

Alisema tatizo la watumishi karibu litamalizika,kulikuwa na idadi kubwa ya watumishi hewa hivyo walikuwa wakiisafisha watumishi hao na hivi karibuni watafungua ajira mpya baada ya zoezi hilo kukamilika.

Samia aliipongeza Chalinze kumaliza tatizo la madawati ila kwenye mafanikio kunajitokeza tatizo jingine hasa kutokana na idadi ya wanafunzi imekuwa kubwa na kuzalisha tatizo la madarasa .

Aliwataka viongozi wa wilaya na mkoa kuelekeza nguvu zao kujenga ,kuongeza na kukarabati majengo ya madarasa  ili watoto waweze kusoma .

Kuhusiana na ahadi ya ujenzi wa soko na stend mjini Chalinze,amemuagiza mkuu wa mkoa huo,mhandisi Evarist Ndikilo kuhakikisha anasimamia hatua ya tathmini ya eneo lililopatikana kwa ajili ya ujenzi huohadi ifikapo mwezi novemba mwaka huu.

Viwanda na uwekezaji,anasema serikali kwasasa inasuka nguvu za viwanda na uwekezaji mkoani hapo kujenga kwa ajili ya kutengeneza ajira na kukuza uchumi wa mkoa .

Alisema viwanda vikubwa 10 vitajengwa ikiwemo cha chuma na nondo,cha kutengeneza vigae na kusindika matunda  hivyo wananchi wawe tayari kupokea wawekezaji ili kupunguza tatizo la uhaba wa ajira.

Akiwa Mlandizi ,Samia aliahidi kuweka uzio kama alivyoahidi wakati wa kampeni kwenye uchaguzi uliopita katika kituo cha afya Mlandizi  kwani ni moja ya sifa ya kuandishwa kwa kituo cha afya kupanda hadhi ya wilaya na bado wanania ya kupandisha hadhi ya kvituo mbalimbali ili kuzipunguzia mzigo hospitali za rufaa .

Alisema soko la mlandizi bado ni dogo ila ana taarifa kuwa kwenye eneo la Kisabi A na B kuna maeneo yamepimwa kwa ajili ya masoko na Tamisemi wameweka mkono kidogo na kuwahakikishia kuwa atakaa na Tamisemi kuangalia uwezekeno wa kuachia maeneo hayo ili kuwepo na soko na stend kubwa .

Alieleza kupimwa kwa mji wa Mlandizi na kusema  ataongea na wizara ya ardhi na sasa bahati nzuri  wizara hiyo  wamekuwa wepesi kufanya zoezi hilo hivyo ataweka msukumo kwa wizara ili waweze kupimiwa na  barabara ya Mlandizi-Mzenga ahadi ipo palepale itajengwa kwa kiwango cha lami .

No comments:

Post a Comment