Sunday, October 16, 2016

Dr. Shein: Hatutakubali misaada yenye masharti

Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein amesema serikali ipo madhubuti katika kupembua misaada ambayo wahisani mbalimbali wapo tayari na katika misaada ambayo itakuwa na masharti magumu kwa sasa serikali haipo tayari kuipokea kwa manufaa ya wananchi.

Dkt. Shein aliyasema hayo juzi  katika sherehe za kilele cha mbio za Mwenge zilizofanyika kitaifa katika mkoa wa Simiyu na kuhudhuriwa na viongozi wa serikali na taasisi binafsi pamoja na mamia ya wananchi pamoja na watoto wa halaiki waliopamba shughuli hiyo.

“Serikali kwa sasa tumejipanga vizuri hatutakubali misaada yenye masharti magumu na wahisani ambao wanataka kufanya hivyo wakae na misaada yao tutajitegemea wenyewe” Alisema Dkt. Shein.

Aidha Rais Dkt. Shein aliwataka watanzania kuendelea kuiunga mkono serikali kwa kuwa imedhamiria kufanya kazi kwa juhudi zote na kusema kwamba ambao wamezoea kuchukua rushwa ni bora waache kwa kuwa serikali haitawavumilia.

Mbio za Mwenge mwaka huu zilifikia tamati baada ya kukimbizwa katika mikoa 31, halmashauri 179 na siku 179 ambapo zimezindua miradi 1,387 yenye thamani ya shilingi bilioni 498.8.

Mbio za Mwenge wa Uhuru mwakani zitazinduliwa mkoani Katavi na kuzimwa mkoani Mjini Magharibi visiwani Zanzibar.

No comments:

Post a Comment