Mgogoro unaoiandama CUF huenda ukailetea balaa zaidi, baada ya kuwapo kwa taarifa kuwa huenda ikafutwa kama itazidi kukomalia msimamo ilionao wa kutotaka ushauri.
Mgogoro huo umekipasua chama hicho na kuwa makundi mawili, moja likiongozwa na Profesa Ibrahim Lipumba na jingine likiwa chini ya Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad.
Profesa Lipumba aliyevuliwa uanachama na Baraza Kuu la Uongozi amejitwalia ofisi kuu za chama hicho zilizopo Buguruni jijini Dar es Salaam, wakati Maalim Seif na wanaomuunga mkono wako makao makuu ya chama hicho Vuga visiwani Zanzibar.
Msajili Msaidizi Sisty Nyahoza kupitia mahojiano yake na kituo cha Channel Ten, ametumia nafasi hiyo kumtambua Profesa Lipumba kuwa bado ni mwenyekiti halali wa CUF na kwamba ofisi hiyo inayo mamlaka ya kukifuta chama chochote.
Alipoulizwa kuwa migogoro hii inayoendelea haiwezi kusababisha chama kikafutwa, Nyahoza amesema vipo vyama viwili vilivyowahi kufutwa usajili wake kwa sababu ya migogoro ya uongozi na kuvitaja vyama hivyo kuwa ni chama cha Pona kilichofutwa Mei 2001.
“Kilikuwa na mgogoro wa uongozi, ambao ulifanya washindwe kufanya uchaguzi wa viongozi wa kitaifa, kingine ni chama cha TPP, vilifutwa kwa hivyo migogoro inaweza ikavunja chama na kikafutwa,” amesema.
No comments:
Post a Comment