KAMPUNI ya Simba Motors imesema ina mpango wa kujenga kiwanda cha kuunganisha magari aina ya pick-up ambacho kitaanza kuzalisha magari kabla ya Desemba 30, mwaka huu.
Ahadi hiyo imetolewa jana mchana (Jumatatu, Oktoba 10, 2016) na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Bw. Jitesh Ladwa mbele ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika mazungumzo yaliyofanyika ofisini kwake Magogoni, jijini Dar es Salaam.
“Tumeamua kuunda magari aina ya pick-up kwa sababu ya mahitaji makubwa yaliyopo nchini. Takwimu zinaonyesha kuwa, kwa mwaka Tanzania inanunua magari ya aina hii zaidi ya 4,000. Katika nchi za SADC mahitaji ni pick-up 35,000 kwa mwaka. Tutaanza na mtaji wa dola za Marekani milioni 200 na tumeomba ekari 200 katika eneo la EPZ,” amesema.
“Eneo la kiwanda cha kuunganisha magari peke yake linahitaji ekari 50, kwa hiyo tukiweka na yadi za kupaki magari, eneo la viwanda vingine, eneo la kushusha na kupakia makontena yatakayokuwa yakisafirishwa kwenda nchi jirani, ni lazima tutahitaji eneo kubwa zaidi,” amesisitiza.
Amesema mradi huo wa majaribio, utaanza kwa kutengeneza magari 20 kila mwezi na kwamba kazi ya utengenezaji magari itaongezeka na kufikia 1,000 na baadaye 5,000 kwa mwaka. “Tunataraji gari la kwanza litazinduliwa kabla ya Krismasi, mwaka huu,” amesema.
Bw. Ladwa amesema uundaji wa magari hayo aina ya Foton-Tunland utafanyika kwa ubia baina ya kampuni yao, SUMA-JKT na kampuni Foton International ya China kwa kutumia teknolojia ya Kichina na kwamba magari hayo yanayotumia 4-Wheel Drive, yana uwezo wa kupita kwenye barabara za aina zote.
Akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Kampuni hiyo, Bw. Aatish Ladwa, amesema mradi utakapoanza, mbali ya kutoa ajira kwa Watanzania, utawezesha pia kujengwa kwa viwanda vingine vitakavyotengeneza matairi ya magari, vioo, taa, bumpers, viti na filters.
“Tunataraji kujenga uwezo wa wahandisi wazawa, uhamishaji wa ujuzi kwa mafundi wa Kitanzania (technology transfer), kupunguza bei kwa mlaji wa mwisho, kupunguza gharama za uzalishaji, kutekeleza amza ya Serikali ya kuifanya Tanzania kuwa ni nchi ya viwanda, kuongeza ajira kwa wanajeshi, na kuwezesha upatikanaji wa vipuri vya magari kwa urahisi na kupunguza uagizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi.”
“Kiwanda kitaajiri wafanyakazi 1,500 kwa kuanzia ambao watakuwemo mafundi na watoa huduma mbalimbali, lakini katika kipindi cha miaka mitatu hadi mitano, tunataraji kuongeza wafanyakazi wengine 5,000 wakati uzalishaji ukiwa umepamba moto,” amesema.
Kwa upande wake, akizungumza mara baada ya kulikagua gari la mfano aina ya Foton-Tunland, Waziri Mkuu amesema anawakaribisha kwenye uwekezaji huo hasa ikizingatiwa kuwa magari hayo yana uwezo wa kupita kwenye maeneo ya vijijini ambako barabara zake siyo nzuri.
“Ofisi za Serikali zinayahitaji zaidi haya magari, hospitali zetu za wilayani nazo pia zinayahitaji haya magari ili yaweze kutoa huduma za chanjo kwa watoto, huduma za UKIMWI, kampeni za kupambana na malaria, na huduma kwa mama wajawazito huko vijijini,” amesema.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
No comments:
Post a Comment