Nchi hizo zimeshindwa kufikia muafaka juu ya namna ya kufufua makubaliano ya kusitisha mapigano Syria. Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani, John Kerry, sasa aelekea kukata tamaa kuhusu amani kurejea.
Hayo yamejitokeza katika Syria mkutano ambao mwakilishi wa Umoja wa Mataifa katika mzozo wa Syria Stefan de Mistura ameuita wenye machungu, mgumu na wenye kukatisha tamaa.
Kundi la kimataiafa linaloiunga mkono Syria, ikiwemo Marekani, Urusi na mataifa mengine yenye nguvu, lililikutana kandoni mwa mkuno wa mwaka wa Umoja wa Mataifa, unaowakutanisha viongozi wa ulimwengu mjini New York wakati jeshi la Syria likiwa limetangaza kuanza mashambulizi mapya ya kijeshi katika eneo linalodhibitiwa na waasi mjini Aleppo.
Kauli ya kukata tamaa ya Kerry
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani John Kerry amesema amesema amekatishwa tamaa, na kwamba ari yake katika mazungumzo imepungua, ikilinganishwa na siku iliyotangulia.
Lakini mwenzake wa Urusi Sergei Lavrov amesema upinzani nchini Syria unapaswa kuchukua hatua katika kufikia makubaliano. Kerry anasema Marekani na washirika wake ambao wanayaunga mkono makundi ya upinzani wako tayari kurejea katika mazungumzo lakini pale tu Urusi itaonesha nia thabiti ya kutekeleza makubaliano ya kuweka chini silaha.
Mashambulizi zaidi Aleppo
Ndege za kivita zimefanya mashambulizi makali katika wilaya zinazodhibitiwa na waasi nchini Syria na kufifisha matumani ya kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoanza 2011. Maafisa kwa upande wa uasi wanasema mabomu ni miongoni mwa silaha zilizovurumisha mjini Aleppo.
Hamza al-Khatib, mkurugenzi wa hosiptali moja katika eneo ambalo linadhibitwa na waasi upande wa mashariki wa mji huo anasema watu 45 wameuwawa.
Katika hatua nyingine Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeipa timu ya uchunguzi ya kimatiafa wiki tano zaidi kukamilisha ripoti yake itakayoeleza nani anayestahili kubeba lawama kufuatia mashambulizi ya gesi ya sumu nchini Syria kitendo ambacho Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ufaransa, Uingereza na mataifa mengine yanasisitiza adhabu kali kwa wale waliohusika na kitendo hicho.
Timu hiyo ilipaswa kuwasilisha ripoti yake juma hili, lakini Ban aliyaambia mataifa 15 wanachama katika barua yake ambayo shirika la habari la Reuters limeiona kwamba waandaaji wanahitaji muda wa ziada na kutaka icheleweshwe hadi Oktoba 21. Baraza limeongeza muda huo mpaka Oktoba 31.
Ripoti ya hivi karibuni kabisa ya baraza la usalama la umoja wa matiafa iliyotolewa mwezi uliopita juu ya uchunguzi wa shirika la umoja huo lenye kudhibiti silaha za kemikali OPCW inaeleza kuwa serikali ya Syria ilihusika na mashambulizi mawili ya gesi ya sumu na Kundi la Dola la Kiislamu lilitumia aina nyingine ya gesi ya sumu. DW
No comments:
Post a Comment