Thursday, September 22, 2016

TTCL NA TPDC ZATOA MILIONI 30 KUSAIDIA WAATHIRIKA TETEMEKO KAGERA

 Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salim Kijuu akipokea msaada uliotolewa na Bodi ya TPDC (kushoto). Kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya TPDC Balozi Dkt. Ben Moses msaada ambao unalenga kuwasaidia kurekebisha makazi ya waathirika wa tetemeko hilo lililoukumba mkoa huo.Picha na Eleuteri Mangi, MAELEZO, Bukoba.

 Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salim Kijuu (kulia) akimshukuru Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) Kamugisha Kazaura (kushoto) mara baada ya kupokea msaada wa mifuko 600 ya saruji ambayo ni sawa na tani 30 yenye thamani ya Sh. milioni 10.
Na Eleuteri Mangi, MAELEZO, Bukoba.
Wafanyakazi na Uongozi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) wametoa msaada wa Sh. milioni 20 kusaidia kununua vifaa vya ujenzi kwa waathirika wa tetemekola ardhi mkoani Kagera.
Akikabidhi msaada huo kwa Mkuu wa Mkoa wa huo Meja Jenerali Mstaafu Salim Kijuu, Mwenyekiti wa Bodi ya TPDC Balozi Dkt. Ben Moses amefafanua kuwa msaada huo unalenga kuwasaidia kununua mabati na saruji kwa waathirika wa tetemeko hilo lililoukumba mkoa huo.
“Sisi TPDC tunatoa msaada wetu kama sehemu ya Watanzania na tatizo hili ni letu sote na Watanzania ni wamoja” alisema Dkt. Moses.
Kwa upande wake Meja Jenerali Mstaafu Kijuu amewashukuru TPDC kwa mchango wao na kubainisha kuwa hakuna kitu kidogo katika kutoa na kuwahakikishia wadau wote wanaotoa michango yao kuwa misaada hyote inayotolewa itatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na itasaidia kuwarudishia makazi waathirika wa tetemeko hilo.
Aidha, Mkuu huyo wa mkoa amewataka watu wote wenye mapenzi mema kuendelee kuwachangia waathirika wa tetemeko hilo na waige mifano ya watu na taasisi mbalimbali wanaoendelea kutoa misaada kwa mkoa wa Kagera ili kuwarudishia makazi wananchi walioathirika maafa hayo.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa TPDC Kapuulya Musomba  amesema kuwa huo sio mwisho wao katika kuchangia waathirika wa tetemeko la ardhi, bali wanaendelea kuwahamasisha wadau wa mafuta na gesi yakiwemo makampuni ya ndani na nje ya nchi ili kuwafanya wananchi waweze kuendelea na kazi zao za kila siku kwa maendeleo yao na taifa kwa ujumla.
Wakati huo huo Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) nao wametoa msaada wa mifuko saruji 600 ambayo ni sawa na tani 30 yenye thamani ya Sh. milioni 10 ikiwa ni mchango wa wa kampuni hiyo katika kuwashika mkono na kuwafuta machozi wananchi wa Kagera. (P.T)

No comments:

Post a Comment